Maandamano Tanzania: Fahamu jinsi Mahakama ya ICC inavyofanya kazi

S

Chanzo cha picha, ICC

Wiki hii Muungano wa kimataifa wa wanasheria na makundi ya haki za binadamu umeiomba rasmi Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) kumchunguza rais wa Tanzania, na serikali yake kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu unaodaiwa kufanywa wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Okyoba 29,2025.

Waraka wenye kurasa 82 kwenda ICC unamtuhumu Rais Samia Suhulu Hassan na maafisa wengine wa ngazi za juu kuhusiana na vifo vya raia wakati wa maandamano ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Hata hivyo idadi ya waliopoteza maisha haijafahamika mpaka sasa, pamoja na kuhuzunishwa na yaliyotokea na akisema ni doa kwa Tanzania, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameunda tume huru ya uchunguzi kuhusu vurugu hizo. Alisema kilichotokea hakikutarajiwa.

Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba akizungumza na wahariri wiki hii kuhusu kilichotokea amesema "Hili jambo halipaswi watanzania kutufikisha kwenye kuuana, sote tunakubalina kwamba wahalifu wanatakiwa wakamatwe, tumejiwekea sheria, kama tunaona utaratibu tunaotumia umetufikisha kutoaminiana, kuleta taharuki, ndiyo maana Mheshimiwa Rais ameunda tume, (kutafuta majawabu)

Ingawa kilichofanya na wanasheria na makundi ya haki za binadamu ni hatua za awali, ni muhimu kufahamu kuhusu Mahakama hii.

ICC imeanzishwa lini na kwanini?

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ni chombo cha kudumu cha kimataifa kilichoanzishwa mwaka 2002 ili kushughulikia uhalifu mkubwa wa kimataifa.

Mahakama hii ina uwezo wa kuwashtaki watu binafsi, wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu, kwa uhalifu kama mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita. ICC ni mahakama ya mwisho, ikingilia kati pale mamlaka za taifa fulani haiwezi au haichukui hatua kwa makusudi kushughulika na uhalifu dhidi ya binadamu na kuhakikisha hakuna mtu aliye juu ya sheria.

ICC ilianzishwa kufuatia vita vya Yugoslavia na mauaji ya Rwanda mwishoni mwa miaka ya 1990. Kabla ya ICC, mahakama za muda za dharura zilijaribu kushughulikia uhalifu mkubwa wa kimataifa, lakini hazikuweza kutoa suluhisho la kudumu.

Mkataba wa Roma, uliosainiwa na nchi 124, ndio msingi wa ICC. Nchi kama Marekani haijajiunga, huku mataifa makuu kama China, India na Urusi yakihofia ushawishi wa kisiasa au uwezekano wa mashtaka dhidi ya wanajeshi au viongozi wake.

Utaratibu wa mashataka na kesi ICC

ICC huchunguza tu pale ambapo mamlaka za taifa hazianzishi ama kutekeleza mashtaka kwa usahihi. Kesi zinaweza pia kupelekwa kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwendesha mashtaka wa ICC, anayejulikana kama Prosecutor, anaweza kuanzisha uchunguzi na mashtaka, lakini yote yanapaswa kuidhinishwa na majaji. Kisha jopo la majaji husikiliza mashahidi na ushahidi kabla ya kutoa hukumu.

Ikiwa mshtakiwa anathibitishwa ama kukutwa na hatia, ICC inaweza kutoa kifungo cha jela, faini au adhabu nyinginezo zinazokubalika kisheria.

Hata hivyo, ICC haina polisi wake, hivyo inategemea mamlaka za kitaifa kushirikiana katika kukamata na kupeleka washukiwa The Hague, Uholanzi, ilipo Mahakama hiyo.

Kesi maarufu zilizowahi kuendeshwa na ICC

A

Chanzo cha picha, VOA

Maelezo ya picha, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya wakati huo akihudhuria kesi yake ICC huko The Hague.

Kesi zilizojulikana za ICC zinaonyesha namna mahakama hii inavyofanya kazi.

Hukumu ya kwanza ilitolewa mwaka 2012 dhidi ya Thomas Lubanga, kiongozi wa wanamgambo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) , aliyetumia watoto katika vita. Rais Uhuru Kenyatta na msaidizi wake William Ruto walifikishwa katika Mahakama hii kwa makosa dhidi ya ubinadamu.

Rais wa zamani wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo, alishtakiwa kwa mauaji, ubakaji na mateso ya raia wake. Joseph Kony, kiongozi wa Lord's Resistance Army wa Uganda, anasakwa kwa uhalifu wa kivita na utekaji nyara wa watoto.

Omar al-Bashir, rais wa Sudan, alisakwa kwa mauaji ya halaiki na uhalifu wa kivita. Hata Rais wa Urusi Vladimir Putin na Kamishna wa Haki za Watoto Maria Lvova-Belova walishtakiwa mnamo 2023 kwa kuhamisha watoto wa Ukraine kinyume cha sheria.

Mipaka na changamoto za Mahakama hii ya ICC

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mahakama ina mipaka kadhaa. Haiwezi kushughulikia uhalifu uliotokea kabla ya 1 Julai 2002, wakati Mkataba wa Roma ulipoanza kutumika. Mamlaka yake inahusiana na nchi zilizoidhinisha mkataba huo, au pale ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapeleka kesi.

Hii inamaanisha kwamba ICC haiwezi kuingilia kati mashtaka yanayoshughulikiwa kikamilifu na mamlaka ya taifa.

Kama nchi husika inayashughulikia kikamilifu madai ya kihalifu, Mahakama hii hukaa pembeni, lakini kama haiyashughulikii kikamilifu, huingilia kati.

Mpaka sasa, baadhi ya mataifa makuu kadhaa hayajajiunga, jambo linalochangia changamoto za kifedha na uendeshaji.

ICC imekosolewa sana kama inawalenga zaidi viongozi wa Afrika pekee, jambo ambalo Umoja wa Afrika limekuwa likilihoji. Hata hivyo, mahakama inasema kesi nyingi ziliwasilishwa na mataifa yaliyoathirika au kupitia Umoja wa Mataifa.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa ushirikiano wa baadhi ya mataifa makubwa. Kesi ya Omar al-Bashir inaonyesha changamoto hii, ambapo Afrika Kusini ilikataa kumkamata licha ya kuwa na hati ya ICC. Marekani haijajiunga, jambo linalochangia changamoto za kifedha na uendeshaji wa mahakama.

Hata hivyo pamoja na changamoto hizi, ICC inabaki chombo cha kipekee cha kimataifa. Mahakama hii inaziba pengo katika mfumo wa haki, kuhakikisha kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria, ikiwemo viongozi wakuu wa nchi, pale ambapo uhalifu mkubwa unafanyika. ICC inaendelea kuwa nguzo muhimu ya kisheria katika kudhibiti mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya binadamu, na uhalifu wa kivita duniani, huku ikikabiliana na changamoto za kisiasa na kifedha.

Zinazovuma zaidi

  1. 6
    Je,ndoa inafaa kuwa na siri?
Morty Proxy This is a proxified and sanitized view of the page, visit original site.