Outer Hebrides

Outer Hebrides au Western Isles, ambavyo wakati mwingine huitwa Long Isle au Long Island, ni mfululizo wa visiwa vilivyopo nje kidogo ya pwani ya magharibi ya nchi kavu ya Uskoti. Huu ndio mnyororo mrefu zaidi wa visiwa katika funguvisiwa la Britania. Visiwa hivyo ni sehemu ya funguvisiwa la Hebrides, na vimetenganishwa na nchi kavu ya Uskoti pamoja na visiwa vya Inner Hebrides na maji ya bahari ya Minch, Little Minch, na Bahari ya Hebridi. Visiwa vya Outer Hebrides vinachukuliwa kuwa ndio kitovu cha asili cha lugha ya Kigaeli cha Uskoti.
Visiwa 19 vinavyokaliwa na watu vilikuwa na makadirio ya wakazi 26,020 mnamo 2024 huku kukiwa na zaidi ya visiwa 50 vikubwa ambavyo havina watu. Umbali kutoka kule Barra Head hadi kilele cha Butt of Lewis ni takriban kilometre 210 (mi 130). Visiwa hivyo ni moja kati ya maeneo 32 ya utawala nchini Uskoti, na tangu mwaka 1998 vimekuwa vikitumia jina la Kigaeli pekee, hata katika mazingira ya Kiingereza. Eneo hili la utawala linaitwa Na h-Eileanan an Iar ('Visiwa vya Magharibi') na baraza lake ni Comhairle nan Eilean Siar.
Jiografia
[hariri | hariri chanzo]

Visiwa hivi vimejipanga kuanzia visiwa vikuu vya Lewis na Harris, North Uist, Benbecula, South Uist, na Barra. Kisiwa cha Lewis and Harris kina ukubwa wa square kilometre 2 178.98 (sq mi 841)[1] na ndicho kisiwa kikubwa zaidi nchini Uskoti na cha tatu kwa ukubwa katika funguvisiwa zima la Britania baada ya Britania na Eire.[2] Upande wa kaskazini unaitwa Lewis na kusini ni Harris, na ingawa mara nyingi huchukuliwa kama visiwa viwili tofauti, vimeungana kwa nchi kavu.[3]
Visiwa vikubwa vimeingiliwa sana na mikono ya bahari kama vile Loch Ròg na Loch nam Madadh. Pia kuna zaidi ya maziwa 7,500 ya maji baridi (lochs) katika Outer Hebrides, ambayo ni takriban 24% ya maziwa yote ya Uskoti.[4] Maziwa kama Loch Langavat kule Lewis yana urefu wa kilometre 11 (mi 7) na yana visiwa vidogo ndani yake. Ziwa la Loch Sgadabhagh kule North Uist linasifika kwa kuwa na umbo tata na la ajabu kuliko ziwa lolote lile nchini Uingereza. Ziwa la Loch Bì ndilo kubwa zaidi kule South Uist na lina urefu wa kilometre 8 (mi 5) kiasi kwamba linakaribia kukigawa kisiwa hicho vipande viwili.
Visiwa vingi vimeundwa na miamba ya kale ya metamofiki[5], na hali ya hewa hapa ni ya wastani na yenye unyevunyevu wa baharini.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Kuna majengo muhimu sana ya kihistoria (historia ya awali) ambayo mengi yalikuwepo hata kabla ya waandishi wa Kirumi na Kigiriki kuanza kuviandika visiwa hivi.
Baadaye, visiwa hivi vilikuwa sehemu ya ufalme wa Wanorway (Norse) uitwao Suðreyjar, uliodumu kwa zaidi ya miaka 400, mpaka mamlaka yake yalipohamishiwa Uskoti kupitia Mkataba wa Perth mwaka 1266. Baada ya hapo, udhibiti wa visiwa ulishikiliwa na machifu wa koo mbalimbali, wakiongozwa na koo za MacLeods, MacDonalds, na MacNeils. Kipindi cha kufukuzwa kwa watu (Highland Clearances) katika karne ya 19 kiliacha makovu makubwa, na ni katika miaka ya hivi karibuni tu ambapo idadi ya watu imeanza kutulia. Leo hii, ardhi nyingi inamilikiwa na jamii za wenyeji wenye asili ya hapa, na uchumi unategemea utalii, kilimo kidogo cha crofting, uvuvi, na ufumaji wa nguo.
Usafiri wa baharini ni kitu cha kufa na kupona kwa watu wa hapa, na kuna huduma nyingi za vivuko kati ya visiwa na nchi kavu. Mifumo ya kisasa ya uongozi wa vyombo vya baharini imepunguza hatari, lakini zamani bahari zenye dhoruba za hapa zilizamisha meli nyingi. Lugha ya Kigaeliki, dini, muziki na michezo ni sehemu muhimu ya maisha yao, na kuna maeneo mengi yaliyohifadhiwa ili kulinda mazingira ya asili.
Asili ya jina
[hariri | hariri chanzo]Maandishi ya kwanza kabisa yaliyobaki yakitaja visiwa hivi yaliandikwa na Plinio Mzee katika kitabu chake cha Natural History, ambapo anasema kuna visiwa 30 vya Hebudes, na kuitaja kando Dumna, ambayo mtaalamu Watson (1926) anasema bila shaka ni Outer Hebrides. Miaka 80 baadaye, mnamo mwaka 140–150 BK, Ptolemy naye alitofautisha kati ya Ebudes (ambavyo alisema viko vitano tu, pengine akimaanisha Inner Hebrides) na Dumna.[6][7] Jina Dumna linaendana na neno la kale la Kiceltic dumnos linalomaanisha "kisiwa cha bahari kuu".[7] Inawezekana Pliny alipata habari zake kutoka kwa Pytheas aliyekitembelea visiwa vya Uingereza kati ya mwaka 322 na 285 KK. Breeze pia anahisi kuwa Dumna inaweza kuwa ni visiwa vya Lewis and Harris, kisiwa kikubwa zaidi katika Outer Hebrides.[6] Watson (1926) anasema maana ya jina la Ptolemy Eboudai haijulikani vizuri na inaweza kuwa ya asili ya kale sana kabla ya Kiceltic.[8]
Pia kuna simulizi za kale za Kieire zinazotaja watu wa Nemed waliokimbilia mahali paitwapo Domon. Katika hadithi za kale za Eire, visiwa hivi vilikuwa makazi ya viumbe wa ajabu walioitwa Fomorians, walioelezwa kuwa "wakubwa na wabaya" na maharamia wa baharini walioitesa pwani ya Eire.[9]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Haswell-Smith (2004) p. 262
- ↑ Haswell-Smith (2004) p. 502
- ↑ Thompson (1968) p. 13
- ↑ "Botanical survey of Scottish freshwater lochs"
- ↑ Miamba ya metamofiki (kwa Kiingereza: metamorphic rocks) ni aina ya miamba ambayo imebadilika kutoka hali yake ya asili kwenda hali nyingine mpya kutokana na shinikizo kubwa (pressure) na joto kali (heat).
- 1 2 Breeze, David J. "The ancient geography of Scotland" in Smith and Banks (2002) pp. 11–13
- 1 2 Watson (1926) pp. 40–41
- ↑ Watson (1926) p. 38
- ↑ Watson (1926) pp. 41–42 quoting Lebor na hUidre and the Book of Leinster.